MKUU wa Wilaya ya Hanang’ atoa onyo

MKUU wa wilaya ya Hanang, Mkoani Manyara, Bi Sara Msafiri amepiga marufuku kufanya shughuli za kibiashara za mazao nje ya soko la Kimataifa la ENDAGAW.

Mkuu wa wilaya hiyo ametoa agizo hilo kwenye uzinduzi wa Bodi ya soko hilo uliofanyika katika Mji wa Katesh na kusema kuwa uchunguzi wa muda mrefu umebaini kuwa idadi kubwa ya wafanyabiashara wamekuwa wakiwadhulumu wakulima kwa kununua mazao yao kwa bei ya chini kwa lengo la kukwepa ushuru wa serikali kwa kuyafuata mazao kwa wakulima.

Awali katika taarifa ya soko hilo iliyosomwa kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Hanang, na Kaimu Afisa Kilimo, Umwagiliaji na Ushirika, Minde Nanagi amefafanua kuwa soko hilo limegharimu zaidi ya shilingi bilioni moja na limeshaanza kutoa huduma kwa majaribio tangu msimu wa mazao mwaka jana

Kwa upande wao baadhi ya wananchi wa Mji wa Hanang, wameonyesha kufurahishwa na uzinduzi wa Bodi ya soko hilo na kwamba hivi sasa wamekuwa na uhakika wa kuuza mazao yao katika soko hilo la Kimataifa la Endagaw.

Wananchi hao wamesema awali kabla ya kuwepo kwa soko hilo wafanyabiashara waliokuwa wakinunua mazao wilayani humo walikuwa wakiwatapeli.

Soko hilo la Kimataifa la Endagaw limejengwa kwa fedha kutoka Benki ya Maendeleo ya Afrika(A.D.B.) kwa kushirikiana na Mfuko wa Kimataifa wa Maendeleo ya Kilimo (IFAD) likiwa na uwezo wa kuhifadhi zaidi ya tani 2,500

About RHN 87.5FM

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *