Janeth Masaburi Aapishwa Rasmi Kuwa Mbunge  

Spika wa Bunge, Job Ndugai amemuapisha  Janeth Masaburi kuwa mbunge. Janeth aliingia bungeni akisindikizwa na wabunge wanawake wa CCM.

Rais John Magufuli, Oktoba 21,2017 alimteua Janeth kushika wadhifa huo.
Janeth ni mke wa marehemu Dk Didas Masaburi aliyewahi kuwa Meya wa Jiji la Dar es Salaam.
Katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015, Dk Masaburi aligombea ubunge wa Ubungo na kushindwa na Saed Kubenea wa Chadema.
Uteuzi wa Janeth umefanywa na Rais Magufuli kwa mujibu wa Ibara ya 66 (1)(e) ya Katiba ya Tanzania inayompa mamlaka ya kuteua wabunge 10 na ulihitimisha nafasi hizo.
Wateule hao ambao ni mawaziri ni; Dk Philip Mpango (Fedha na Mipango), Profesa Palamagamba Kabudi (Katiba na Sheria), Profesa Joyce Ndalichako (Elimu, Sayansi na Teknolojia), Profesa Makame Mbarawa (Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano) na Dk. Augustine Mahiga (Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa).
Wengine walioteuliwa na Rais Magufuli ni Dk Tulia Ackson ambaye ni Naibu Spika wa Bunge, Salima Kikwete, Anne Kilango na Abdallah Bulembo.