Tuhuma kwa Meya – Iringa

Meya wa Manispaa ya Iringa, Alex Kimbe amepewa siku tano kujibu tuhuma zinazomkabili ikiwamo matumizi mabaya ya madaraka.

Hatua hiyo imefika baada ya wajumbe 19 wa Baraza la Madiwani la manispaa hiyo, kusaini maombi wakitaka kifanyike kikao maalum cha kujadili kumng’oa madarakani.

Kulingana na barua iliyosainiwa Jumatatu, Machi 2, 2020 na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Iringa, Hamid Njove meya huyo anatakiwa kuwasilisha utetezi wake kwenye ofisi za mkurugenzi huyo ndani ya siku tano kuanzia jana.

Makosa manne anayotuhumiwa nayo Meya huyo  wa Manispaa ya Iringa, Alex Kimbe (CHADEMA):
1. Matumizi mabaya ya madaraka.
2. Matumizi mabaya ya rasilimali za halmashauri.
3. Mwenendo mbaya au ukosefu wa adabu.
4. Kushiriki katika vitendo vya rushwa .